Politics Social

Mizengo Pinda akelwa na Jina la Zuzu

Imeandikwa na Admin

#WAZIRI Mkuu mstaafu #MizengoPinda ameiomba serikali kubadilisha jina la Kijiji cha Zuzu ambacho anaishi.

Aidha, Pinda ameiomba serikali kukiita kijiji hicho Zinje, akieleza kuwa jina hilo la sasa halina maana nzuri katika Kamusi ya Kiswahili; ikizingatia wakazi wa eneo hilo ni wachapakazi.

Pinda aliyasema hayo juzi wakati Mwenge wa Uhuru ulipowasili kijijini hapo na kutembelea miradi ya kilimo na ufugaji anayoiendesha kwa kushirikiana na wakazi wa eneo hilo.

Kiongozi huyo alisema amejaribu kutafuta maana ya jina hilo kwa kuandika ‘zuzu’ katika mtandao na kubaini lina maana mbaya na katika ufuatiliaji wake aliona kuna neno ‘zinje’ ambalo alidai linastahili kuwa jina la kijiji hicho kwa kuwa lina maana inayoakisi shughuli zinazofanyika ndani ya eneo hilo.

“Nimejaribu kutafuta neno hilo la zuzu na kuona lina maana mbaya, ndiyo maana nimeomba pabadilishwe na kuitwa Zinje ambayo ina maana fulani ndani ya eneo hili,” alisema Pinda.

Alisema ‘zinje’ ina maana ya jiwe laini ambalo hupatikana maeneo hayo na wazee wa zamani walikuwa wakilitumia kutengeneza kiko cha kuvutia tumbaku.

Pinda alifichua maombi yake yanaelekea kukubalika baada ya Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Jordan Rugimbana kuanza kulifanyia kazi suala hilo.

Akizungumzia kuhusiana na kazi za kilimo cha zabibu, nyanya, pilipili hoho na vingine ambavyo analima, Pinda alisema anashukuru Mungu vinaendelea vizuri kutokana na kilimo cha kisasa anachofanya.

Alisema kilimo ni kazi nzuri kama itaifanyika kwa ufasaha huku akiwataka watu wajitokeze kupata elimu ya kilimo katika shamba darasa ambalo analiendesha katika eneo hilo la Zuzu.

Alisema ni vema jamii ikazingatia suala zima la kilimo na ufugaji kwa sababu vinatengeneza ajira kubwa na ya uhakika kwa wananchi kuanzia hatua ya awali hadi kuvuna.

Kiongozi wa Mbio za Mwenge Kitaifa, Amour Hamad Amour, alisema kuna kila sababu ya wananchi kwenda kujifunza suala la kilimo katika shamba darasa la kiongozi huyo.

Alisema Pinda anastahili pongezi kwa sababu amefanya kazi kubwa ya kuendesha kilimo na kutoa mafunzo kwa wengine wanaopenda kujifunza kilimo na ufugaji wa nyuki na mifugo mingine.

Kutokana na jitihada zake hizo, Pinda alikabidhiwa cheti cha pongezi kama ishara ya kazi nzuri ya ufugaji na kilimo ambayo anaifanya katika shamba hilo.

Mkuu wa Wilaya ya Dodoma, Christine Mndeme, aliitaka jamii ijitokeze kwa wingi kwenda kujifunza kwa Pinda kwa kuwa anaendesha kilimo chenye tija, ikiwamo kuisaidia jamii.

“Tunaomba jamii ijitokeze kujifunza katika shamba darasa la Pinda, wakifuatilia na kuzingatia maelekezo, watafika mbali katika kilimo,” alisema Mndeme.

Related Post