Entertainment Social

Lulu Anarudi Uraiani, Familia Yake Yapata Tumaini

Imeandikwa na Admin

MWIGIZAJI wa filamu za Kibon­go, Elizabeth Michael maarufu kwa jina la Lulu ana uwezakano mkubwa kurejea tena uraiani endapo atakamilisha mambo matatu ya kisheria.

Siri hiyo imefichuka ikiwa ni siku mbili baada ya Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Dar es Salaam kuamuru atumikie kifungo cha miaka miwili jela kutokana na kumuua bila kukusudia mwigizaji mwenzake, Steven Kanumba maarufu The Great.

Tukio hilo la kusikitisha lilitokea Aprili 7, 2012 nyumbani kwa marehemu Kanumba, Sinza- Vatican, jijini Dar es Salaam.

TUJIUNGE NA MWANASHERIA

Akizungumza juzi na gazeti hili, mwanasheria wa kujitegemea, alisema pamoja na hukumu iliyotolewa, yapo mambo matatu ya kuzingatia kisheria ili kumrejesha Lulu uraiani.

JAMBO LA KWANZA

Mwanasheria huyo ambaye hakupenda kutaja jina lake kutokana na sababu maalumu, alisema jambo la kwanza ni kuhakikisha anatumikia robo ya kifungo chake gerezani (miezi mitano).

JAMBO LA PILI

Jambo la pili awe na uwezo wa kuithibitishia mahakama pasipo shaka yoyote kuwa rufaa atakayokata atashinda na jambo la tatu ni kwa kutumia Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977.

“Haya mambo mawili yakizingatiwa vizuri kisheria Lulu anarudi uraiani kama kawaida, lakini pia anaweza kurejea kwa msaada wa Katiba,”alisema mwanasheria.

KATIBA KIVIPI?

Kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977, ibara ya 45 (1) (a) inasema;

Rais anaweza kutoa msamaha kwa mtu yeyote aliyepatikana na hatia mbele ya mahakama kwa kosa lolote na anaweza kutoa msamaha huo ama bila masharti au kwa masharti, kwa mujibu wa sheria.

Pia ibara hiyo inasema Rais anaweza kumwachilia kabisa au kwa muda maalumu mtu yeyote aliyehukumiwa kuadhibiwa kwa ajili ya kosa lolote ili mtu huyo asitimize kabisa adhabu hiyo au asitimize adhabu hiyo wakati wa muda huo maalumu.

“Rais anaweza kufuta adhabu yoyote au sehemu ya adhabu yoyote aliyopewa mtu yeyote kwa ajili ya kosa lolote au kufuta adhabu yote au sehemu ya adhabu ya kutoza,” ilifafanua zaidi ibara hiyo.

WAKILI AFUNGUKA

Akielezea zaidi suala hilo, Wakili Rosan Mbwambo alisema, Lulu anaweza kukatiwa rufaa Mahakama ya Rufaa Tanzania na akatoka kwa dhamana.

Hata hivyo, alitoa angalizo kuwa ni lazima awe ametumikia robo ya adhabu ya hukumu yake.

Alisisitiza kuwa uamuzi wa Lulu kuwa nje bado utabaki kuwa wa mahakama endapo itajiridhisha na vifungu vilivyokatiwa rufaa.

“Hili la kukatiwa rufaa linawezekana,” alisema na kufanunua kuwa hilo litawezekana kutokana na vigezo na masharti ya mahakama.

KIBATALA

Wakati wakisema hivyo, Wakili wa Lulu, Peter Kibatala alikaririwa Jumatatu iliyopita nje ya Mahakama Kuu akisema anatarajia kukata rufaa Mahakama ya Rufaa Tanzania.

Alipoulizwa atatumia vipengele gani kukataa rufaa hiyo, alisema,“Sasa hivi ni mapema mno, nikishapitia hukumu nitajua ni vipengele gani vya kukatia rufaa.”

FAMILIA YAPATA MATUMAINI

Chanzo kilicho karibu na familia ya Lulu kimeeleza kuwa, baada ya familia hiyo kuelezwa mambo hayo, ilipata matumaini upya.

“Japo kuna process ndefu kidogo na ugumu lakini angalau wameweza kupata tumaini jipya,” kilisema chanzo hicho.

MAHAKAMANI

Jumatatu iliyopita, Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Sam

Rumanyika alimhukumu Lulu kutumikia adhabu hiyo huku mahakama ikiwa imefurika watu wengi.

Baada ya kupitia maelezo ya mashahidi pamoja na kuwasikiliza mawakili wa pande zote mbili, Jaji Rumanyika alisema kifo cha Kanumba kilitokana na ugomvi hivyo amejiridhisha kwamba mtuhumiwa aliua bila kukusudia.

“Sheria ya kuua bila kukusudia inaleta udhibiti kuwa watu wanatakiwa wafanye mambo kwa tahadhari, wivu wa maendeleo huleta maendeleo, wivu wa mapenzi huleta maangamizi,” alisema.

Jaji alisema kuna kitu kikubwa ambacho Lulu anakificha kwa kuwa aliielezea mahakama kuwa Kanumba alikuwa akimpiga kwa bapa la panga lakini yeye hakuweza kusema kama alijitetea au hata kama alitumia msemo wa Biblia ‘akupigae shavu la kulia, mgeuzie na kushoto’, hakueleza hayo.

“Hivyo inaonesha kabisa kuwa hapo kuna kitu fulani alikuwa anakificha kwa makusudi,” alisema jaji huyo.

Baada ya hukumu, vilio vilitawala mahakamani ambapo Lulu alishindwa kujizuia na kuangua kilio, huku mama wa Kanumba, Flora Mtegoa akionekana mwenye tabasamu.

ILIVYOKUWA

Itakumbukwa kuwa marehemu Kanumba alifariki majira ya saa nane usiku, baada ya kutokea ugomvi kati yake na Lulu.

Kanumba alijizolea umaarufu mkubwa katika ukanda wa Afrika Mashariki na Kati hadi Afrika Magharibi baada ya kuwashirikisha katika filamu zake baadhi ya wasanii maarufu wa kutoka nchini Nigeria, akiwemo Mercy Johnson na Noah Ramsey.

Kanumba alizaliwa mwaka 1984 na kuanza kujipatia umaarufu mwanzoni mwa mwaka 2000 wakati huo akiigiza kupitia kundi la maigizo la Kaole Sanaa.

Aliendelea na kuigiza filamu nyingi ambazo zilimpatia umaarufu mkubwa hivyo kusafiri mara kadhaa nchi za nje, ambako alitambulika kama mmoja wa wasanii wenye vipaji vikubwa ambaye aliitangaza fani ya filamu nchini Tanzania maarufu kama ‘Bongo Movies.’

Mazishi yake yalichukua sura ya kitaifa kutokana na umaarufu aliojijengea msanii huyo katika jamii ya Watanzania na hata nchi za nje.

Related Post