Politics Social

Serikali yamtilia shaka Dk. Shika

Imeandikwa na Admin

WAKATI jina la #Dk #LouisShika likiendelea kuibua mijadala kwenye mitandao mbalimbali ya kijamii ikiwamo ya kutaka asaidiwe kisaikolojia ili mwishowe alitumikie taifa, serikali imeonyesha dalili za kutilia shaka kuhusu daktari huyo.

#Dk. #Shika alianza kujipatia umaarufu Novemba 9 mwaka huu wakati aliposhinda katika mnada wa kununua nyumba tatu za kifahari za Lugumi Enterprise zilizopo Upanga na Mbweni jijini Dar es Salaam kwa ahadi yake ya kulipa Sh. bilioni 3.3 kwa nyumba zote, lakini mwishowe akaishia Polisi baada ya kubainika kuwa hana hata senti tano.

Katika mahojiano yake kwenye vyombo mbalimbali vya habari, Dk. Shika alitoa ushuhuda wa kusisimua kuhusiana na maisha yake akiwa Urusi alikokwenda kusoma na baadaye kuishi, na pia namna alivyobobea katika taaluma ya utabibu, akihitimu shahada nne na kufikia ngazi ya kuwa na shahada ya uzamivu ya tiba za binadamu (PhD of Medicine).

Maelezo hayo ya Shika, ambayo amekuwa akiyatoa kwa kujiamini huku pia akithibitisha kwa rejea kadhaa katika simulizi za maisha yake huku akijinasibu kuwa na fedha nyingi kupitia kampuni yake ya Lancefort iliyopo Moscow, Urusi, ndiyo yaliyoibua mijadala kwenye mitandao huku baadhi wakitaka asaidiwe kisaikolojia ili arudi katika hali yake ya kawaida na mwishowe serikali itumie ujuzi wake katika masuala ya afya nchini.

Hata hivyo, akizungumza na Nipashe jana, Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dk. Mpoki Ulisubisya, alionyesha kuwa serikali inatilia shaka juu ya uwezekano huo wa kumtumia Dk. Shika katika masuala ya tiba nchini kwa sasa.

Mwandishi alimhoji Dk. Ulisubisya kuhusiana na kumtambua Dk. Shika na kujua kama serikali inaweza kumsaidia na mwishowe kumwezesha (Dk. Shika) kuifanyia kazi taaluma yake kwa manufaa ya taifa kutokana na elimu kubwa aliyo nayo.

Katika majibu yake, ndipo Dk. Ulisubisya alipoonyesha kuwa na shaka kwa Dk. Shika.

“Kabla ya kujibu swali lako, naomba nikuulize, umeshafika hospitali ya Muhimbili? Pale nje kuna mtu anaimba na kuhubiri, unamjua?” Dk. Dk. Ulisubisya alimhoji mwandishi kabla ya kuongeza:

“Nikirudi kwenye swali lako, utambue kuwa kwenye sekta ya afya… katika fani ya udaktari kuna taratibu zake za kufanya kazi.

Ulitakiwa ufuatilie kwanza ili ujue taratibu kwa sababu ili mtu afikie hatua ya kutibu, anapita katika hatua nyingi, si kwamba mtu akisema tu eti amesomea udaktari basi anakwenda hospitali kutoa tiba. Ziko taratibu ambazo zinapaswa kufuatwa.”

Aidha, Dk. Ulisubisya alimwelekeza mwandishi wa habari hizi kuonana na Mganga Mkuu wizarani ili kumpa taratibu zote za kufuatwa kuajiri madaktari na kama mtu akipata changamoto kama za Dk. Shika anasaidiwa kwa namna gani.

Jitihada za mwandishi kumpata Mganga Mkuu jana zilishindikana baada ya simu yake kuita bila kupatikana.

Katika maelezo yake, Dk. Shika alisema kiweledi yeye ni daktari wa binadamu aliyesomea Urusi na alikwenda huko mwaka 1984 kwa ufadhili wa Wizara ya Afya wakati huo.

Alisema alisoma shahada ya kwanza kwa miaka saba aliyoimaliza mwaka 1991, kisha akaendelea na shahada ya magonjwa ya kuambukiza ambayo alimaliza mwaka 1993.

Dk. Shika alisema shahada ya uzamivu (PhD) aliisomea kwenye chuo kingine kilichopo Moscow, Urusi baada ya kuhama Chechnya kutokana na vita baina ya jimbo hilo na serikali wakati huo.

Alisema baada ya kumaliza PhD, aliendelea na masomo na kuchukua shahada ya nne ya udaktari wa tiba na kwamba mara alipomaliza alifundisha kwenye chuo alichosomea.

Pia alisema mbali na elimu aliyonayo na kufundisha, Julai 28, mwaka 1999 alifungua kampuni yake kwa shughuli za biashara ya Lancefort inayojihusisha na kemikali za viwandani.

Katika baadhi ya mijadala mitandaoni, mmoja wa wachangiaji alidai kuwa huenda hivi sasa Dk. Shika anasumbuliwa na ugonjwa wa Paranoia, ambao mtu huhitaji msaada wa madaktari in gawa kwa watu wa kawaida ni ngumu kujua kuwa ni magonjwa kwa sababu mhusika huwa na uwezo wa kusimulia mambo vizuri tu, na tena kwa mtiririko unaoeleweka (logical sequence).

Wachangiaji wengine walikuwa wakimhusisha na mashirika ya kijasusi ya CIA la Marekani na KGB la Urusi wakati akiwa nje ya nchi na ndiyo maana alipata matatizo hadi kutekwa wakati fulani, madai ambayo mwenyewe amekaririwa akiyakanusha na kusisitiza kuwa aliwahi kutekwa kwa sababu ya kuwa na fedha nyingi.

“ITAPENDEZA ZAIDI” YATIKISA BUNGE
Umaarufu wa ghafla wa Dk. Shika, ambaye anaishi katika chumba kimoja cha kupanga, eneo la Tabta jijini Dar es Salaam, ulijidhihirisha bungeni mjini Dodoma juzi wakati kauli yake maarufu ya “Itapendeza zaidi” ilipotamkwa na Spika wa Bunge, Job Ndugai. Vishindo vya shangwe na vicheko vya wabunge viliibuka ghafla wakati kauli hiyo ilipotamkwa wakati wa kupitisha vifungu vilivyokuwa kwenye Muswada wa Sheria ya Wakala wa Meli wa mwaka 2017.

Awali, Dk. Shika alitoa kauli hiyo kwa mara ya kwanza katika mnada mmojawapo wa nyumba za Lugumi Novemba 9, pale aliposema “Mia tisa itapendeza zaidi”, akimaanisha kuwa yuko tayari kulipa Sh. milioni 900 na mwishowe akawashinda wapinzani wake waliokuwa tayari kulipa Sh. milioni 810.

Namna ilivyokuwa, ni kwamba Spika Ndugai ambaye katika kikao hicho alikuwa mwenyekiti baada ya Bunge kuketi kama kamati, alikuwa akiwahoji wajumbe kwa kutamka ‘kifungu hicho kinaafikiwa?’

Alipofikia kifungu cha 61 cha muswada huo, ndipo Ndugai alipowaacha hoi wabunge baada ya kusema: “kifungu cha 61 itapendeza zaidi.”

Baada ya kuona bunge limelipuka kwa shangwe na vicheko, Spika alisema kwa utani, “huo msemo wa Wasukuma (Dk. Shika ni Msukuma), tuendelee waheshimiwa…kifungu cha 61 kinaafikiwa?”

UMAARUFU
Siku ya mnada Novemba 9, Dk. Shika alikuwa ni miongoni mwa mwa watu waliojitokeza kwa nia ya kutwaa nyumba hizo.

Kila mara wakati watu wengine walipojaribu kupanda bei ya kununua nyumba hizo, Dk. Louis alinyoosha mkono na kutaja dau la juu zaidi kiasi kwamba wote aliwashinda kirahisi, hali iliyowafanya wafanyakazi wa kampuni ya udalali ya Yono wampepee na kumshangilia kwa ushindi wake.

Baada ya kuibuka kidedea kwenye mnada huo, alipotakiwa kutoa asilimia 25 ya fedha za nyumba alizoshinda, Dk. Shika aliwaacha midomo wazi waendesha mnada baada ya kubainika kuwa hana fedha, huku akisema kuwa angeweza kutoa siku moja au mbili mbele kwa sababu hatembei na fedha mfukoni.

“Tatizo ni kutoelewana, nyumba zinauzwa na wametaka nilipe asilimia 25 zilipwe siku hiyo hiyo na hapo hapo na mimi fedha zangu ziko nje, hapo ndipo tuliposhindwana,” alisema Dk. Shika wakati alipoulizwa juu ya kile kilichotokea.

Hatua ya Dk. Shika kushindwa kulipa asilimia 25 kama alivyotakiwa ilisababisha Jeshi la Polisi kumweka mbaroni ambapo alikaa mahabusu kwa siku sita hadi alipoachiwa juzi kwa dhamana na sasa amekuwa akiripoti kila siku katika Kituo Kikuu cha Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam.

Hadi kufikia jana, Dk. Shika aliendelea kuwa maarufu mtandaoni huku miongoni mwa picha zake zinazowavutia wengi kwenye mitandao ya kijamii ni ile aliyokalia tofali akinywa chai kwa mama lishe na nyingine akiwa amesimama ndani ya daladala.

Pia katika baadhi ya picha za utani mitandaoni, picha za Dk. Shika zilikuwa zikiunganishwa na za matajiri mbalimbali duniani pamoja na watu maarufu, akiwamo tajiri namba moja, Mmarekani Bill Gates.

*Imeandikwa na Romana Mallya (Dar) na Athanas (Dodoma)

Related Post