Business Politics Social

KAULI YA MBUNGE YADAIWA KUCHOCHEA WANANCHI KUUA TEMBO

Imeandikwa na Admin
KAULI za baadhi ya #wanasiasa za kuhamasisha wananchi kuua tembo katika Jimbo la Serengeti mkoani Mara zinadaiwa zimeanza kuleta athari baada ya watu wanne kukamatwa na #Polisi kwa tuhuma za kuua tembo.
Baadhi ya wananchi ambao wameomba majina yao kutoandikwa kwenye habari hii, wameiambia Michuzi Globu kwa njia ya simu kuwa kuna mbunge wa Jimbo la Serengeti Marwa Chacha(Chadema) akiwa kwenye msiba wa kijana mmoja mwenye umri wa miaka 32 aliyeuliwa na tembo katika kijiji cha Kenoku kwa Mfano aliwaambia wananchi hao kuwa Serikali imeshindwa kuweka uzio ili tembo wasilete madhara, hivyo nao wawaue tembo tu.
Kwa mujibu wa watoa taarifa hizi wamedai baada ya kauli hiyo imeonekana kuchochea watu kufanya ujangiri kwa kuua tembo na Jumatano ya wiki hii kuna watu wanne katika kijiji cha Robanda wamekamatwa kwa tuhuma za kuua tembo.
“Ni vema Mbunge akawa makini na kauli zake kwani baada ya kuwaambia wananchi waue tembo wanapokuja kijijini, tayari kuna watu wanne wamekamatwa kwa tuhuma za kuua tembo eneo la kijiji cha Robanda jimboni Serengeti.“Hili si la kulifumbia macho kwa mbunge wetu amekuwa na utamaduni wa kutoa kauli ambazo zinachangia wananchi kuua tembo”amedai moja ya watoa taarifa hizi.
MBUNGE AFAFANUA
Akizungumza na Michuzi Globu, Mbunge wa Serengeti Chacha Marwa amesema madai ya wananchi hao ambao wametoa taarifa hizo hayana ukweli wowote.
Kwani amesema hakuna mahali ambako amewaambia wananchi waue tembo na badala yake amekuwa akiiomba Serikali kufanya jitihada za kuweka uzio ili tembo wasiingie vijijini kwa wananchi kwani watu wanakufa na mazao yanaharibiwa kila kukicha.Marwa amesema amefuatilia suala hilo muda mrefu Wizara ya Maliasili na Utalii tangu Waziri akiwa Profesa Jumanne Maghembe lakini hakuna uzio hadi leo hii.
Ameongeza amewahi kuandika barua kwa Spika wa Bunge ya kulalamikia tembo kuingia maeneo ya wananchi na kuleta madhara hakuna ambacho kimefanyika.“Nikweli nilienda kushiriki kwenye msiba wa kijana mmoja aliyeuliwa na tembo siku za karibuni, ila sijahamasisha wananchi kuua tembo na siwezi kufanya hivyo.
 
“Kwanza kijiji ambacho msiba umetokea ni kilometa 50 na kijiji cha Robanda, sasa kwanini wanizushie hayo maneno.Hayo ni mambo tu ya siasa za huku kwetu.“Pia tuseme ukweli, wananchi wamekuwa wakiteseka sana kutokana na tembo kuja kwenye makazi ya watu na kuleta madhara, kila siku wananchi wanalia na ipo siku watachoka kweli.
“Hivyo niiombe Serikali itusaidie kuondoa tatizo hili huku kwetu kwa kulinda usalama wa wananchi wake,”amesema Marwa.
POLISI YATAJA WANAOSHIKILIWA
Jeshi la Polisi Mkoa wa Mara limekiri kukamatwa kwa watu hao baada ya kupatikana kwa taarifa za kuua tembo hao ambapo kwa sasa jeshi hilo linawashikilia. 
Limewataja watuhumiwa wanaoshikiliwa kwa kutuhuma hizo za kuua tembo na kukutwa wakiwa na meno yake ni Kirihena Bwanana(34),mkazi wa Bwitenga.Wengine ni Kasimu Mussa(40),mkazi wa Robanda, Hamisi Gamuhu(37),mkazi wa Robanda na Hamisi Mabula(52) mkazi wa Kitembele.
 Watuhumiwa wa pembe za ndovu wakiwa wamewekwa chini ya ulinzi mara baada ya kunaswa wakituhumiwa kuua tembo.
 Mtuhumiwa wa pembe za ndovu akiwa amewekwa chini ya Ulinzi na Askari Wanyama Pori  

 

Mtuhumiwa wa pembe za ndovu akiwa amewekwa chini ya Ulinzi na Askari Wanyama Pori  

Related Post