Politics Social

lissu alivyopaa dk. 500 ulaya

Imeandikwa na Admin

HATIMAYE Mbunge wa Singida Mashariki (Chadema) na Rais wa Chama cha Mawakili wa Tanganyika (TLS), #Tundu #Lissu, amesafiri jana kutoka nchini Kenya kuelekea katika nchi ya Ubelgiji barani Ulaya kwa ajili ya kupatiwa matibabu zaidi.

Kwa mujibu wa mtandao wa masuala ya safari za ndege wa prokela (www.prokerala.com), wastani wa safari ya moja kwa moja ya ndege kutoka Nairobi hadi jijini Brussels, Ubelgiji huchukua saa nane na dakika 25, sawa na dakika 505; hiyo ikitokana na wastani wa umbali mfupi kwa njia ya anga wa kilomita 6,570 kutoka Nairobi hadi Ubelgiji.

Hata hivyo, taarifa ambayo Nipashe ilithibitishiwa jana, ilieleza kuwa safari hiyo ya Lissu ilianzia jana hiyo saa 2:30 asubuhi kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Jomo Kenyatta, kwa ndege ya Shirika la Kenya na itapitia Uholanzi kabla ya kufika Ubelgiji.

Taarifa hiyo ilileza kuwa katika safari hiyo, Lissu ameongozana na mkewe Alicia. Alisindikizwa kutoka Hospitali ya Nairobi alikolazwa tangu Septemba, kuelekea uwanja wa ndege na watoto wake pacha, Augustino na Edward, ndugu zake na pia baadhi ya viongozi wa juu na makada wa Chadema, ambao ni pamoja na Mwenyekiti Freeman Mbowe, Katibu Mkuu Dk. Vicent Mashinji, Naibu Katibu Mkuu Bara, John Mnyika na Visiwani Zanzibar, Salum Mwalimu. Wengine ni Mbunge Tarime Vijijini John Heche, Susan Kiwanga (Mlimba), Godbless Lema (Arusha Mjini), Rose Kamili (Viti Maalum), Anna Gideria (Viti Maalum) na ndugu wengine.

Taarifa zaidi kutoka Nairobi zilieleza kuwa, Lissu akiwa uwanja wa ndege, mbali na kuwashukuru madaktari wa hospitali ya Nairobi na wale wa mkoani Dodoma, alisema anakwenda kupatiwa matibabu Ubelgiji na kwamba takaporudi, mapambano (ya kudai haki) yataendelea.

“Nikirudi mapambano yanaendelea. Nawashukuruni nyote mlioniombea, nawashukuru Wakenya na serikali yao ambao kwa miezi minne nikiwa hapa walinipa ulinzi wakati wote. Chapeni kazi, mimi nitarudi kuendeleza mapambano haya,” Lissu alikaririwa akisema.

Chanzo kutoka TLS kiliiambia Nipashe jana kuwa, akiwa Ubelgiji, Lissu atakuwa chini ya uangalizi maalum ulioratibiwa na kamati inayoratibu matibabu yake.

Alisema pia wamewasiliana na serikali ya nchini humo kwa ajili ya kumpatia ulinzi wakati wote akipatiwa matibabu katika moja ya hospitali kubwa nchini humo.

Hata hivyo, chanzo hicho hakikuwa tayari kutaja mji wala hospitali atakayofikia na kulazwa kwa ajili ya matibabu yake.

“Kwa sasa ni mapema kutaja mji anaoenda. Isipokuwa atakapowasili Ubelgiji, atakuwa akiangaliwa kwa ulinzi binafsi na wakati wote akiwa hospitalini hapo. Lakini pia tumeshazungumza na serikali ya nchi hiyo kwa ajili ya ulinzi zaidi,’ kilieleza chanzo hicho, kikigusia hofu itokanayo na mazingira ya mkasa wa Lissu kushambuliwa kwa risasi zaidi ya 20 na watu wasiojulikana Alhamisi ya Septemba 7, mwaka jana wakati akiwa katika eneo analoishi Area D mjini Dodoma.

Katika hatua nyingine, chanzo hicho kilieleza kuwa tayari kumeanza kuwapo na matumaini makubwa ya kuondolewa kwa risasi moja iliyonasia kwenye nyonga ya Lissu kutokana na matibabu atakayopata akiwa Ubelgiji.

Wakati akizungumza na waandishi wa habari jijini Nairobi juzi, Lissu alisema kuwa risasi moja imebaki mwilini na madaktari kumshauri abaki nayo kwakuwa ni hatari kuiondoa, huku risasi nane zikiondolewa na madaktari waliomhangaikia kuokoa maisha yake katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Dodoma na nyingine saba zikitolewa na madaktari wa hospitali ya Nairobi.

Chanzo kiliiambia Nipashe kuwa mbali na kuwapo kwa matumaini ya kuondolewa kwa risasi hiyo moja, akiwa Ubelgiji, Lissu ataangaliwa zaidi pia maendeleo ya operesheni 17 alizofanyiwa na mwishowe, atafanyishwa mazoezi ya viungo ili aimarike zaidi.

MBWANA SAMATTA

Nchi aliyokwenda kutibiwa Lissu ya Ubelgiji, ndiko alipo Mbwana Samatta ambaye ni mshambuliaji na nahodha wa timu ya taifa, Taifa Stars.

Samatta anaichezea klabu ya Genk iliyopo umbali wa barabara wa kilomita 83 kutoka katika mji mkuu wa nchi hiyo wa Brussels ambao ndiyo Lissu anatarajiwa kutua na ndege akitokea Uholanzi.

“Kama Lissu atakuwa akitibiwa katika mji wa Brussels, maana yake bado atakuwa jirani tu na mji aliopo Samatta… umbali kati ya miji hiyo haufiki kilomita 100,” chanzo kiliifafanualia Nipashe, kikimtaja Samatta kwa nia ya kuwawezesha Watanzania wengine waweze kukumbuka vyema nchi aliyokwenda Lissu kutibiwa.

Related Post