Social

Mvua kubwa ilivyotikisa Jiji Dar

Imeandikwa na Admin

MVUA kubwa iliyonyesha jana jijini Dar es Salaam imesababisha athari katika maeneo kadhaa ikiwamo wananchi kukosa makazi na kusitishwa kwa muda kwa usafiri wa mabasi yaendayo haraka, maarufu Mwendokasi.

Waliokosa makazi ni wanaoishi maeneo ya mabondeni kutokana na mvua hiyo kuzingira makazi hayo.

Aidha, barabara kadhaa zilizingirwa na maji kutokana na mitaro kujaa, hivyo kusababisha msongamano wa magari kwa saa kadhaa baada ya mvua hiyo kuanza majira ya alfajiri.

Msongamano wa magari ulisababisha usumbufu mkubwa kwa watu waliokuwa wanakwenda kazini, sehemu za biashara, maeneo mengine na wanafunzi waliokuwa wanakwenda shuleni.

Pia, baadhi ya wakazi walilazimika kuzikimbia nyumba zao baada ya kuzingirwa na maji bila kujua hatima yao.

Kaimu Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Benedict Kitalika, aliwataka wakazi wa mabondeni kuhama mara moja kutoka maeneo hayo bila kusubiri kukumbwa na mafuriko.

Kamanda huyo alisema ni hatari watu kuendelea kuishi katika maeneo hatarishi wakisubiri kuondolewa na serikali, badala yake wahame haraka kunusuru maisha yao na wasirudi tena katika maeneo hayo.

SITISHA HUDUMAAwali jana asubuhi, Kampuni ya Mabasi Yaendayo Haraka (Udart) kupitia kwa Mkuu wake wa Kitendo cha Mawasiliano, Deus Bugaywa, ilitangaza kusitisha kwa muda huduma zake kutokana na kujaa maji juu ya daraja la Mto Msimbazi kwenye barabara ya Morogoro na kusababisha kufungwa kwa barabara hiyo.

“Tunauarifu umma kuwa huduma za mabasi hayo zimesitishwa kwa muda kuanzia saa 3:00 asubuhi. Mara baada ya hali kutengemaa na mamlaka husika kuruhusu barabara hiyo kuendelea kutumika, huduma zitarejea mara moja,” alisema Bugaywa.

Imekuwa ni kawaida Jiji la Da es Salaam kukumbwa na mafuriko mvua zinaponyesha na pia wakazi wa mabonde ambao hukumbwa na mafuriko wamekuwa wakihama kwa muda kisha hurejea upya katika makazi yao kinyume cha wito wa kila mara wa kuwataka kuondoka katika maeneo hayo hatarishi.

Serikali imekuwa ikitupiwa lawama kwa kuruhusu ujenzi holela katika maeneo hayo, ingawa ilishawahamisha kutoka mabondeni, lakini baadhi yao wakaamua kurudi kuendelea na maisha.

Miongoni mwa mafuriko makubwa yaliyowahi kulikumba jiji hilo ni ya Desemba 20, 2011 ambayo yaliacha vifo vya zaidi ya watu 40 na uharibifu wa mali ambapo serikali ilichukua hatua za dharura kuhakikisha huduma za chakula, malazi na mavazi zinapatikana kwa waathirika wa mafuriko hayo.

Related Post