Politics

Saa 96 hatima uwaziri wa Kairuki, Dk. Tizeba

Imeandikwa na Admin

UTEUZI wa mawaziri wawili na manaibu wao uko hatarini kutenguliwa baada ya jana Rais John #Magufuli kuweka wazi kutoridhishwa na utendaji kazi wao na kuwaagiza kutekeleza maagizo mazito ndani ya saa 96 kuanzia jana.

Waziri wa Madini, #AngellahKairuki (KUSHOTO) na waziri wa Kilimo Dk. #CharlesTizeba

Wizara zilizotajwa moja kwa moja na Rais Magufuli kuongozwa na mawaziri ambao wameonekana kutokwenda sambamba na kasi yake ya uongozi, ni Wizara ya Madini na Wizara ya Kilimo.

Wizara ya Kilimo inaongozwa na Dk. Charles Tizeba akisaidiwa na Mary Mwanjelwa wakati Wizara ya Madini inaongozwa na Angellah Kairuki akisaidiana na Stanslaus Nyongo na mwishoni mwa wiki Rais Magufuli aliongeza naibu waziri wa pili, Doto Biteko.

Akimwapisha Bitoke jana Ikulu jijini Dar es Salaam, Rais Magufuli aliweka wazi kwamba hajaridhishwa na utendaji kazi wa Wizara ya Madini ambayo ni mpya ndiyo maana ameamua kumwongeza Biteko ambaye aliongoza kamati maalum iliyoundwa na Bunge kwa ajili ya kuchunguza tanzanite mwanzoni mwa mwaka wa fedha 2017/18.

Rais aliiagiza wizara hiyo kwa kushirikiana na Wizara ya Katiba na Sheria kuhakikisha kanuni za sheria mpya ya madini Na. 7 ya mwaka 2017 zinasainiwa kufikia Ijumaa.

Alibainisha kutoridhishwa kwake na namna viongozi na watendaji wa Wizara ya Madini wanavyotekeleza majukumu yao polepole na bila kujali maslahi ya nchi.

“Sheria hii imepitishwa na Bunge na mimi nikaisaini tangu mwezi wa saba (Julai) mwaka 2017, mpaka leo (jana) ni miezi 7 bado hamjasaini kanuni zake ili sheria ianze kutekelezwa, na wahusika wote wapo, yaani mpaka leo hamjaelewa Watanzania wanataka nini?” Rais Magufuli alihoji.

“Ndiyo maana nikamteua aliyekuwa kwenye kamati ya madini, ili labda atatoa changamoto kwa wenzake maana labda yeye anaelewa zaidi.

“Kule kwenye tanzanite mnada ulikuwa ufanyike karibu nusu tani, nikazuia mwishoni usiku kwamba hamuwezi kufanya mnada wa madini karibu nusu tani.

Haya yatanunuliwa kwa ‘value’ (thamani) ya chini, na matapeli watavusha hiyo tanzanite na itaenda na hatuna ‘regulations’ (kanuni).

Nikazuia usiku wa saa sita. Na ndiyo maana nasema sasa hivi mnada hauwezi kufanyika tena mpaka hizi ‘regulations’ zisainiwe.”

Alimwagiza Waziri wa Katiba na Sheria, Prof. Palamagamba Kabudi kushirikiana na Naibu Mawaziri, Katibu Mkuu na Wakurugenzi wanaohusika katika Wizara ya Madini kuhakikisha kanuni hizo zinasainiwa.

Pamoja na maagizo hayo, Rais Magufuli alitangaza kutengua uteuzi wa Kamishna wa Madini, Benjamin Mchwampaka na kumteua Prof. Shukrani Manya kuwa Kamishna wa Madini na pia kukaimu nafasi ya Mtendaji Mkuu wa Kamisheni ya Madini.

Kabla ya uteuzi huu Prof. Manya alikuwa Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) Idara ya Jiolojia.

Aliwataka viongozi kushughulikia maeneo yao kwa kiwango kikubwa akisisitiza kuwa kiongozi anapokumbushwa mabaya kwenye eneo lake na yeye yupo, afikirie kwamba halimudu anatakiwa yeye mwenyewe agundue kabla wengine hawajagundua.

Alisema kuna changamoto ya baadhi ya watumishi na wataalamu wa Wizara ya Madini kuchakachua kanuni kwa kupunguza mambo wanayoona yanaharibu maslahi yao.

“Kwa sababu wapo wengine wana hisa kwenye kuchimba madini huko, wengine ni ‘share holders’ (wanahisa), wapo wengine wana leseni za uchimbaji, wengine ni za ndugu zao na wengine majina yapo kwa ndugu zao,” Rais alisema.

“Mimi si mwanasiasa mzuri wa kubembeleza bembeleza, nikitoka mimi mtapata wa kubembeleza, ila mimi nataka kabla ya Ijumaa ‘regulations’ hizo ziwe zimesainiwa. Prof. Kabudi nendeni mkazifanyie kazi tafuta watu wa kukusaidia na mkamalize hayo.

“Isije ikawa kila mtu anayepelekwa Wizara ya Madini pafanane kama kuna pepo fulani linawabadilisha akili mnaenda… kwa sababu kule kuna hela na dhahabu nazo ni kama mapepo tu, inawezekana yanawaharibu akili huko halafu hamchukui ‘decision’ (uamuzi) vizuri kwa sababu ukute huku kuna dhahabu, ukigeuka huku kuna tanzanite inaning’inia, huku kuna almasi.”

“Mpaka sasa hivi tangu sheria hii ipitishwe, Wizara ya Madini ‘haijani-impress’ (haijanikosha) na mumfikishie salamu hizi waziri bado hajani-impress. Lakini ‘I hope’ (natumaini) mtabadilika.”

TIZEBA MTEGONIRais Magufuli pia aliiagiza Wizara ya Kilimo inayoongozwa na Dk. Tizeba kuhakikisha mbolea inafikishwa katika mikoa yote ya uzalishaji wa chakula ukiwamo mkoa wa Rukwa kufikia Ijumaa.

Jana Nipashe iliripoti kuhusu tishio la kutokea kwa baa la njaa mkoani Rukwa mwaka huu kutokana na changamoto ya upatikanaji wa mbolea mkoani humo.

Katika maagizo yake, Rais alimwelekeza Waziri Mkuu Kassim Majaliwa kufuatilia jambo hilo huku akibainisha kuwa endapo mbolea haitafikishwa katika maeneo hayo kufikia Ijumaa wahusika waachie ngazi.

“Wakulima wanataka mbolea na muda ni huu, inasikitisha sana fedha kwenye bajeti zimetengwa, lakini mpaka leo (jana) mbolea haijawafikia wakulima. Sasa mkoa kama Rukwa ndiyo tunaoutegemea kwa chakula, waziri yupo na watendaji wake wapo lakini mpaka leo mbolea haijapelekwa, wakulima watazalishaje chakula?” Alihoji Rais Magufuli.

MAKONTENA 178 MAKINIKIAAliwataka watendaji wote wa serikali kutekeleza majukumu yao ipasavyo na kuonya kuwa hatosita kumfukuza kazi mtendaji yeyote atayeshindwa kutekeleza wajibu wake kwa maslahi ya Watanzania.

“Nataka kila mmoja afanye kazi, Watanzania wanataka maendeleo, hakuna muda wa kubembelezana, kila mmoja afanyie kazi mambo yanayomhusu asisubiri kuambiwa, kule bandarini niliunda timu za kuchunguza madudu yaliyopo huko naambiwa kuna makontena 178 ya makinikia hayana mwenyewe, mengine yapo Ubungo, mengine bandari,” aliongeza.

Rais Magufuli pia alimpongeza Spika Job Ndugai na wabunge kwa kazi nzuri wanayozifanya zikiwamo kamati zinazoundwa kuchunguza mambo mbalimbali na kukiri kuwa Bunge limekuwa likiisaidia sana serikali kukabiliana na changamoto mbalimbali.

Hafla ya kuapishwa kwa Biteko ihudhuriwa na Spika Ndugai na viongozi mbalimbali wa wizara na vyombo vya ulinzi na usalama.

Baada ya kuapishwa Biteko alimshukuru Rais Magufuli kwa uteuzi na kumwahidi kufanya kazi kwa bidii.”Niko tayari kufanya kazi kwa bidii na namwomba Mungu usije jutia uamuzi wako,” Biteko alisema.

Related Post