Kwetu Bongo

Online Magazine

Mtanzania aripotiwa kufa maji Marekani

MWANAFUNZI Mtanzania Allen Buberwa (22) aliyekuwa akisoma chuo nchini Marekani, ameripotiwa kufa maji katika mto Buffalo uliopo Pruitt Jimbo la Arkansas.

Taarifa za Serikali ya Jimbo la Arkansas, imethibitisha tukio hilo na kueleza kuwa Buberwa aliyekuwa akisoma Chuo cha North Arkansas katika Mji wa Newton, alifikwa na umauti Jumatatu jioni wiki hii baada ya kuzama kwenye kina kirefu cha mto huo. Taarifa hiyo ya serikali imefafanua kuwa Buberwa, alikuwa akiogelea katika eneo maarufu la kuogelea kabla ya kuzama katika kina kirefu na kufa.

Wazamiaji waliupata mwili wa Buberwa Jumatatu hiyo saa tano usiku (kwa muda wa Marekani). Alikuwa katika programu ya wanafunzi wa Kimataifa katika chuo hicho. Mamlaka zilipewa taarifa ya tukio hilo saa 12 jioni (kwa saa za Marekani) wakati Buberwa na watu wengine watatu walipoonekana wakijaribu kuogelea katika mto huo kuelekea katika eneo jingine la mto.

Taarifa ya serikali inasema Buberwa alionekana kuogelea kwa tabu na alifika eneo lenye kina kirefu na alipozama ndani ya maji, hakuibuka tena. “Waogeleaji wenzake hawakufanikiwa kumuokoa,” ilieleza taarifa hiyo. Kwa mujibu wa taarifa ya Serikali ya Newton iliyotolewa na kiongozi wa eneo hilo, Glenn Wheeler, maofisa wa serikali walielezwa na mashuhuda kuwa Buberwa aliteleza na kutumbukia katika mto huo kwenye eneo la kina kirefu na mtu mmoja alipiga mbizi kumuokoa, lakini wote walionekana kuhangaika kujiokoa.

“Hata hivyo, mashuhuda wametueleza kuwa watu wawili walizamia kwenye maji na kufanikiwa kumuokoa yule mti alutejitupa ili kumuokoa Buberwa na Buberwa alipotelea majini na mwili wake uliibuliwa saa tano baada ya kuzama,” alisema Wheeler katika taraifa yake.

“Tukio hili ni baya na la kuhuzunisha, tunaiombea familia yake na marafiki,” alisema Wheeler na kuongeza kuwa, tukio hilo limekatisha ndoto ya kijana huyo mdogo aliyekuwa akisoma katika Chuo cha North Arkansas karibu na Harrison. Mwakilishi wa chuo alichokuwa akisoma mwanafunzi huyo alikuwa eneo la tukio kushiriki kumtafuta na alikuwa akiwasiliana na familia ya Buberwa iliyopo nchini Marekani na Tanzania.

Wheeler alisema waokoaji kutoka Ofisi ya Newton, Huduma za Hifadhi za Jamii, BUFFSAR, Kitengo cha Majanga cha Mennonite, taasisi za kidini, Kitengo cha Zimamoto na Uokoaji cha Harrison, Kituo cha Afya cha Arkansas (EMS), Kikosi cha Msalaba Mwekundu cha America na vikosi vingine vya zimamoto kutoka maeneo mbali mbali walishiriki kutafuta mwili wa Buberwa.

Mto huo upo umbali wa kilometa 169 kaskazini magharibi mwa mji maarufu wa Little Rock. Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki ilipoulizwa jana kuhusu tukio hilo, ilisema inafuatilia kupata uhakika wake na itaujulisha umma wa Watanzania.

Kakobe: Ukimgusa mmoja, umetugusa wote
MAKONDA AWAOMBA MSAMAHA WACHAGA, ASKOFU AMPATANISHA NA MBOWE
Recommended
x