Isabel dos Santos: Mfanyakazi wa benki apatikana amefariki mjini Lisbon

0
156

Mwanamke tajiri zaidi barani Afrika Isabel dos Santos

Mfanyakazi mmoja wa benki anayehusishwa na kesi ya ufujaji na ulanguzi wa fedha dhidi ya mwanamke tajiri barani Afrika, Isabel dos Santos amepatikana amefariki mjini Lisbon.

Nuno Ribeiro da Cunha mwenye umri wa miaka 45 alisimamia akaunti za kampuni ya mafuta Sonangol, ambaye mwenyekiti wake alikuwa bi Dos Santos katika benki ya EuroBic nchini Ureno.

Kifo chake siku ya Jumatano kiliripotiwa siku ya Alhamisi muda mfupi tu baada ya waendesha mashtaka nchini Angola kuwataja wote wawili kama washukiwa.

 • Mali ya mwanamke tajiri zaidi Afrika yakamatwa
 • Mwanamke tajiri Afrika afunguliwa mashtaka ya ulaghai
 • Benki ya Ulaya yakata uhusiano na mwanamke tajiri Afrika

Bi Dos Santos amekana madai ya ufisadi yaliofichuliwa na stakhabadhi zilizovuja.

Bwana Da Cunha alipatikana amefariki katika mojawapo ya mali zake mjini Lisbon. Chanzo kimoja cha polisi kiliambia chombo cha habari cha Portugal kwamba huenda mshukiwa huyo alijiua.

Vyombo vya habari nchini humo vilinukuu polisi wakisema bwana Da Cunha alikuwa tayari amejaribu kujiua mwezi huu na kwamba alikuwa akiugua shinikizo la akili.

Siku ya Jumatano Eurobic ilisema kwamba itasitisha uhusiano wake wa kibiashara na bi Dos Santos ambaye ameripotiwa kuwa mwanahisa mkuu wa benki hiyo kupitia kampuni mbili anazomiliki.

Baadaye iliripotiwa akisema kwamba bi Dos santoa atauza hisa zake katika benki hiyo.

Benki hiyo pia ilisema kwamba itachunguza uhamisho wa fedha usio wa kawaida unaohusisha makumi ya mamilioni ya madola ambayo zilikuwa katika akunti yake.

Baadhi ya fedha hizo zilifilisi akaunti ya Sonangol katika benki ya EuroBic kulingana na gazeti la New York Times.

Katika taarifa siku ya Alhamisi, bi Dos Santos alielezea madai hayo dhidi yake kama yasio na ukweli wowote.

Je anatuhumiwa na nini?

Waendesha mashtaka wa Angola wanajaribu kukomboa $1bn (£760m) ambazo bi Dos Santos na washirika wake wanadaiwa kulipora taifa hilo.

Isabel dos Santos ametuhumiwa kwa usimamizi mbaya na ufujaji wa fedha wakati alipokuwa mwenyekiti wa Sonangol, alisema mwendesha mashtaka mkuu Helder Pitta Gros ambaye alikuwa akifanya mkutano na wanahabari siku ya Jumatano jioni.

Alisema kwamba kutokana na hilo, atashtakiwa na ulanguzi wa fedha, kutumia ushawishi wake, usimamizi mbaya na kughushi stakhabadhi miongoni mwa uhalifu mwengine wa kiuchumi.

Mamlaka nchini Angola sasa itafanya uchunguzi ili kubaini iwapo atahitajika kushtakiwa . Pia wametaja watu wengine watano akiwemo bwana Ribeiro da Cunha na kuwataka kurudi nchini Angola.

Bwana Pitta Gros alisema kwamba iwapo bi Dos Santos hatorudi kwa kujitolea , agizo la kimataifa la kumkamata litatolewa dhidi yake.

Bi Dos Santos aliteuliwa kwa njia ya utata kuongoza kampuni ya Sonangol mwezi Juni 2016 na babake, aliyekuwa rais wa taifa hilo.

Alifutwa kazi 2017 na aliyemrithi babake, rais Joao Lourenco.

Uchunguzi dhidi ya bi Dos Santos ulianzishwa baada ya mrithi wake katika Songanol Carlos Sturnino , kuelezea mamlaka kuhusu uhamisho wa fedha usio wa kawaida. Mali yake nchini Angola imekamatwa.

Je kuna nini katika stakhabadhi zilizovuja?

Siku ya Jumapili , BBC na mashirika mengine ya habari yaliripoti zaidi ya stakabadhi 700,000 zilizovuja kuhusu biashara za tajiri huyo.

Stakabadhi hizo zilionyesha jinsi bi Dos Santos alivyojipatia mikataba ya ardhi, mafuta, almasi na mawasiliano wakati babake alipokuwa rais.

Mali yake inadaiwa kuwa $2.1 bn (£1.6bn).

Pia zilionyesha jinsi kampuni za magharabi zilivyomsaidia bi Dos Santos kutoa fedha zake nje ya Angola.

Aliyataja madai hayo kuwa ya uongo na kudai kwamba serikali ya Angola inamlenga kisiasa.

Mapema wiki hii , afisa mmoja mkuu wa kampuni ya hesabati PwC alijiuzulu katika kampuni hiyo baada ya kuhusishwa na bi Dos Santos.

Kampuni hiyo ilikataa kutoa tamko lolote na kusema kwamba imeanzisha uchunguzi wake.

Je Dos Santos amesema nini?

Katika taarifa yake siku ya Alhamisi, bi Dos Santos alikana madai hayo akiyataja kuwa mpango wa serikali kumkabili kisiasa kabla ya uchaguzi mkuu wa Angola.

”Pia ni jaribio la kunipunguza nguvu na sifa ya rais Dos Santos na familia yak . Hakuna mtu anayepswa kutekwa na mbinu kama hizo”, alisema. Bi Dos Santos alisema stakabadhi zilizoibwa zilifichuliwa kiubaguzi ili kutoa sura mbaya kuhusu biashara zake.

”Mimi ni mfanyakazi wa kibinafsi ambaye nimehudumia miaka 20 nikijenga biashara zilizofanikiwa kutoka chini, na kubuni ajira 20,000 mbali na kuipatia Angola mapato makubwa kupitia kodi”.

”Nimekuwa nikiendesha biashara zangu kwa kufuata sheria na kwamba biashara zangu zote zimeidhinishwa na mawakili, benki, wakaguzi na wadhibiti sheria”,alisema.

Aliongezea aliwaomba mawakili wake kuchukua hatua dhidi ya habari za uongo na kwamba alikuwa tayari kuikabili kesi hiyo katika mahakama za kimataifa ili kulinda jina lake zuri.

Isabel dos Santos ni nani?

 • Mwana mkuu wa aliyekuwa rais wa taifa hilo Jose Eduardo Dos Santos
 • Ni mke wa mfanyabiashara wa Congo Sindika Dokolo
 • Alihudumu katika shule ya upili ya wasichana ya mabweni nchini England.
 • Alisomea uhandisi wa umeme katika chuo kikuu cha Kings College mjini London.
 • Akiwa na miaka 24 alikuwa akimiliki hisa katika mgahawa wa Miami Beach uliopo mjini Luanda
 • Aliinuka na kuwa mwanamke tajiri zaidi barani Afrika
 • Alichaguliwa kuongoza shirika kuu la mafuta nchini Angola la Sonangol 2016 na kufutwa kazi 2017.
 • Ana hisa za asilimia sita katika mafuta ya Ureo na kampuni ya gesi ya galp ambayo ni thamani ya $830m
 • Anamiliki 42.5% ya benki ya Portugal ya Eurobic bank
 • Ana asilimia 25% ya hisa katika kampuni ya simu ya Unitelnchini Angola
 • Pia ana 42.5% ya hisa katika benki ya Angola kwa jina Banco BIC

Mlipuko wa kirusi cha Corona wazua hofu China