MR NICE AMKABA KOHO HARMONIZE

0
126

Wimbo wake wa Hainistui umemtia matatani tena msanii maarufu Bongo, Rajabu Abdul Kahali a.k.a Harmonize au Harmo.  Kwetu Bongo limenasa skendo mbichi ikidai kuwa Harmo amekopi biti ya wimbo wa King’asti ulioimbwa na mkongwe kwenye game, Lucas Mkenda ‘Mr Nice’ ambaye ameibuka hivi karibuni na malalamiko hayo mazito.

“Harmonize amepiga beats zangu bila idhini yangu, ni kama ameniibia. Ninaumia kwa hili; ni kama mtoto unayempenda kwenye familia yako halafu anakuibia,” alilalamika Mr Nice alipokuwa akihojiwa na mtandao mmoja wa kijamii nchini Kenya ambako hufanya kazi zake za sanaa kwa sasa.

MR NICE ANATAKA NINI?

Ingawa alionesha kukasirishwa na kitendo cha Harmo kukopi kazi yake iliyompaisha mwaka 2006, Mr Nice hakutamka wazi ni hatua gani atazichukua kwa msanii huyo aliyemtuhumu kukopi kazi yake.

Katika maelezo yake kwenye mtandao huo wa kijamii alisema; kwake lisingekuwa jambo baya kama Harmo angemtaarifu tu kuwa anachukua utamu kidogo kwenye ngoma yake ya King’asti kuliko kufanya kimyakimya kwa njia ya wizi.

NI KAMA MARUDIO

Tuhuma hii ya kukopi biti kutoka kwenye kazi za msanii mwingine imekuja kwa Harmo kama mwendelezo wa ile ya kwanza ambapo kwenye wimbo wake wa Uno alidaiwa kunakili mdundo wa wimbo Dundaing wake Magix Enga, mtayarishaji wa muziki nchini Kenya.

Kufuatia madai hayo ya Magix aliyotoa Novemba 17, mwaka jana dhidi ya Harmo, wimbo wa Uno ulilazimika kuondolewa kwa muda kwenye mtandao wa YouTube hadi pale Harmo na Magix walipoweka sawa mgogoro wao.

MENEJA WA HARMO AFUNGUKA

Kufuatia skendo hiyo, mwandishi wetu alimvutia waya Meneja wa Harmo, anayejulikana siku zote kwa jina moja la Mjerumani, kumuuliza nini kinachoendelea nyuma ya pazia la madai hayo mazito ya kukopi kazi ya Mr Nice ambapo alisema:

“Hiyo taarifa ipo na mimi niliiona kwenye mtandao mmoja ila inashughulikiwa lakini siwezi kukuambia imefikia wapi kwa sababu inawahusu watu wawili (Harmo na Mr Nice). Ni jambo la msanii na msanii, sasa sioni kama ni busara kuweka wazi kwenye media (vyombo vya habari).”

Hata hivyo, majibu hayo yalionesha wazi kuwa Harmo kwa mara nyingine ameingia matatani kwa kukopi kazi ya msanii mwenzake bila ruhusa.

DIAMOND ATAJWA

Hata hivyo, penye wengi kuna mengi ambapo baadhi ya mashabiki wamemtaja bosi wa zamani wa Harmo, Nasibu Abdul ‘Diamond’ kuwa ndiye anayechochea skendo za Harmo kukopi nyimbo zionekane ni kitu kibaya kwa lengo la kumvurugia.

“Wasanii wangapi wanakopi nyimbo lakini hakuna kelele kubwa kama anazopigiwa Harmo. “Sema aliowakimbia (huenda anamaanisha kitendo cha Harmo kutoka Wasafi iliyo chini ya Diamond na kuanza kufanya kazi binafsi) ndiyo wanamsukia zengwe ili kumshusha kimuziki,” alisema shabiki mmoja wa Harmo kwenye ukurasa wake wa Facebook.

Itakumbukwa kuwa skendo ile ya kwanza ya wimbo wa Uno ilikuja muda mfupi baada ya Harmo kujitoa Wasafi huku hii ya pili ikijitokeza siku chache baada ya Harmo kutangaza kuwa yuko tayari kufanya kazi na Ali Kiba, hasimu mkubwa wa kimuziki wa Diamond.

Hata hivyo mara kadhaa uongozi wa Diamond umekuwa ukikanusha kuhusika na hujuma zozote kwa Harmo kwa madai kuwa hawana bifu naye. Kwetu Bongo, bado lipo chimbo linamwulika kwa karibu sakata hili na litakuhabarisha kila hatua litakayofikia.

Siri ya Lulu diva kuvaa nusu utupu
Gadget Ogling: Amazon on Fire, Virtual Reality, True Nature and Energy Relief