Nchimbi, Fei Toto watimka Yanga, wapata dili Urabuni

0
270

WACHEZAJI wa Yanga mshambuliaji mpya Ditram Nchimbi na kiungo fundi Feisal Salum ‘Fei Toto’ wiki iliyopita waliondolewa usiku kwenye kambi ya timu hiyo wakakwea ndege kwenda kwenye moja ya klabu nchini Misri kwa ajili ya majaribio.

Wachezaji hao waliondolewa kwenye kambi ya timu hiyo iliyoweka Regency Hotel, Mikocheni jijini Dar es Salaam iliyokuwa inajiandaa na mchezo wa Ligi Kuu Bara dhidi ya Azam FC uliopigwa wikiendi iliyopita kwenye Uwanja wa Taifa.

Nchimbi huenda akawa ameingia Yanga na neema hiyo ikiwa ni siku chache tangu ajiunge na timu hiyo kwenye usajili wa dirisha dogo kwenye msimu huu akitokea Polisi Tanzania alipokuwa anacheza kwa mkopo akitokea Azam FC.

Kwa mujibu wa taarifa ambazo imezipata Championi Ijumaa na kuthibitishwa na Ofisa Habari wa Yanga, Hassan Bumbuli wachezaji hao wapo Misri tangu wikiendi iliyopita wakiendelea na majaribio.

“Hizo taarifa ulizozisikia za kuwahusu Nchimbi na Fei Toto kwenda kufanya majaribio ni kweli kabisa, wachezaji hao wameondoka tangu wiki iliyopita kuelekea Misri walipokwenda katika majaribio.

“Kila kitu kinachowahusu wachezaji hao kitawekwa wazi mara baada ya kukamilika usajili wao na watakuwa huko kwa kipindi maalum ambacho klabu hiyo husika imewaomba,” alisema Bumbuli.